Unguja. Upanuzi wa hospitali na ongezeko la vyumba vya upasuaji Zanzibar vimeongeza uhitaji wa wataalamu wa ganzi na usingizi tiba, huku idadi ya waliopo ikiwa chini ya mahitaji ya mfumo wa afya.
Waziri wa Afya Zanzibar, Nassor Ahmed Mazrui amesema visiwa hivyo vinahitaji takribani wataalamu 400 wa ganzi na usingizi tiba ili kukidhi mahitaji ya vyumba vya upasuaji vilivyopo, vinavyojengwa na vinavyotarajiwa kujengwa.
Hata hivyo, amesema waliopo kwa sasa ni 111, sawa na asilimia 27.75 ya mahitaji yote, hali inayoacha upungufu wa wataalamu 289.
Mazrui ametoa kauli hiyo leo, Oktoba 16, 2026, wakati wa maadhimisho ya Siku ya Ganzi na Usingizi Tiba yaliyoambatana na uzinduzi wa Jumuiya ya Ganzi Zanzibar (Zasa).
Amesema kati ya wataalamu 111 waliopo, ni 53 pekee wanaofanya kazi, sawa na asilimia 13.25 ya mahitaji yote, huku wengine 58 wakiwa masomoni.
“Jambo hili linahitaji uwepo wa mkakati madhubuti wa mafunzo na ajira ili kuhakikisha vituo hivi vyote vina wataalamu wenye uwezo wa kutoa huduma salama,” amesema Mazrui.
Tangu mwaka 2021, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeendelea kuongeza vyumba vya upasuaji na kutekeleza miradi ya ujenzi na upanuzi wa hospitali, ikiwemo Hospitali ya Rufaa Mnazimmoja, Binguni na hospitali za mikoa.
Mazrui amesema ongezeko hilo la miundombinu linapaswa kwenda sambamba na maandalizi ya wataalamu wa kutosha ili huduma za upasuaji zitolewe kwa usalama na ufanisi.
Amesema umefika wakati Chuo cha Afya kuwekwa chini ya usimamizi wa moja kwa moja wa Wizara ya Afya, akieleza kuwa hatua hiyo itaiwezesha Serikali kutumia vizuri wakufunzi na wataalamu waliopo na kupanga mafunzo kulingana na mahitaji halisi ya sekta.
Kwa mujibu wa Mazrui, chuo hicho kina uwezo wa kuzalisha wataalamu 50 kila mwaka, ambao wanaweza kusaidia kupunguza pengo lililopo.
Pia ameiagiza Wizara ya Afya, kwa kushirikiana na Tume ya Utumishi wa Umma, kuharakisha mchakato wa kuitambua taaluma ya ganzi kama kada huru yenye mfumo wa maendeleo ya kikazi.
Kwa upande wake, Daktari Bingwa wa Ganzi na Usingizi katika Hospitali ya Mkoa wa Lumumba, Dk Peter Frank Saria, akisoma risala kwa niaba ya wataalamu, ameiomba Serikali kuongeza ajira na kuboresha vifaa tiba katika hospitali za Unguja na Pemba.
Amesema hatua hizo zitasaidia kupunguza mzigo wa kazi kwa watumishi waliopo na kuimarisha usalama wa wajawazito na watoto wanaofanyiwa upasuaji.
Awali, Daktari Nassra Ishaka Yussuf akiwasilisha matokeo ya tafiti kuhusu afya ya uzazi, amesema shinikizo la juu la damu wakati wa ujauzito linachangia takribani asilimia 20 ya vifo vyote vya wajawazito Zanzibar.
Amesema utafiti uliohusisha wajawazito 728 ulibaini kuwa hali ya preeclampsia huongeza uwezekano wa kujifungua mtoto mwenye uzito mdogo kwa mara 3.8.
Ametumia fursa hiyo kuhimiza jamii kuachana na imani potofu zinazoweza kuwazuia wajawazito kupata huduma za afya na kuwahimiza kuhudhuria kliniki mapema.

