Geita. Wakati matumizi ya kuni na mkaa yakiendelea kuwa juu katika maeneo ya vijijini, Shule ya Sekondari Kalangalala mkoani Geita imepokea kilo 1,500 za mkaa mbadala hatua inayolenga kupunguza utegemezi wa kuni na kuongeza matumizi ya nishati safi.
Msaada huo umetolewa na Geita Gold Mining Limited (GGML) ikiwa ni sehemu ya juhudi za kusaidia shule hiyo kutumia nishati inayolinda mazingira na kupunguza matumizi ya nishati za jadi.
Pia inakwenda sambamba na juhudi za Serikali za kuongeza matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini hasa katika taasisi zinazotumia kiasi kikubwa cha nishati kila siku.
Msaada huo wa kilo 1,500 za mkaa mbadala ni mwendelezo ikiwa ni baada ya Juni 5, 2026, kutoa majiko banifu 240 kwa wananchi mkoani Geita katika maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani.
Ofisa Mwandamizi wa Mazingira wa GGML, Josephine Kimambo amesema matumizi ya nishati safi na endelevu katika shule na taasisi za Geita ni miongoni mwa maeneo ambayo kampuni hiyo imeyapa kipaumbele.
Msaada wa mkaa mbadala uliotolewa na Geita Gold Mining Limited (GGML) ikiwa ni sehemu ya juhudi za kusaidia shule kutumia nishati inayolinda mazingira na kupunguza matumizi ya nishati za jadi.
Amesema wanafunzi wanapotumia teknolojia hizo shuleni, wanapata fursa ya kujifunza umuhimu wa kutunza mazingira na wanaweza kupeleka uelewa huo katika familia na jamii zao.
“Wanafunzi na wafanyakazi wa shule wanapotumia teknolojia hizi moja kwa moja, hujenga uelewa kuhusu umuhimu wa uhifadhi wa mazingira unaokwenda zaidi ya eneo la jikoni,” amesema.
Kwa mujibu wa kampuni hiyo, lengo si kusaidia matumizi ya majiko banifu pekee bali kujenga utamaduni wa matumizi yanayowajibika ya nishati na utunzaji wa mazingira katika taasisi zinazowalea na kuwaandaa vijana.
Tayari Serikali imeweka Mkakati wa Taifa wa Nishati Safi ya Kupikia 2024–2034 unalenga kuongeza matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini hadi kufikia asilimia 80 huku taasisi zinazohudumia idadi kubwa ya watu zikitajwa kuwa muhimu katika kuharakisha mabadiliko hayo.


