Safari ya nishati safi inavyokumbana na mikingamo

Safari ya nishati safi inavyokumbana na mikingamo

‎‎Dar es salaam. Licha ya juhudi za Serikali kuchochea matumizi ya nishati safi ya kupikia, bado kuni na mkaa zinaonekana kuwa chanzo cha kwanza cha nishati kwa Watanzania wengi wanapotaka kupika.

Hilo linathibitishwa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), inayosema asilimia 70 ya Watanzania wanatumia kuni na mkaa kama chanzo cha nishati ya kupikia.

Hali iko hivyo, wakati Serikali imejiwekea lengo la kuhakikisha asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi kupikia ifikapo mwaka 2034, kama ilivyobainishwa katika Mkakati wa Taifa wa Nishati Safi ya Kupikia wa 2024/34.

Kwa mujibu wa baadhi ya wananchi, gharama ndogo na urahisi wa upatikanaji ndizo sababu zinazowafanya wachague kuni na mkaa, badala ya nishati nyingine zinazotajwa kuwa safi, ikiwemo gesi.

Serikali nayo inaeleza kuwa imeamua kuwabana hata katika mkaa, kwa kuongeza bei ya leseni na vibali vya kubeba nishati hiyo kutoka shambani, huku ikifanya juhudi za kuunganisha gesi asilia kwenye makazi ya watu ili kurahisisha upatikanaji wake.

‘Mkaa nafuu, gesi bei juu’

Akizungumza na Mwananchi, mmoja wa watumiaji wa mkaa, Haji Omar anasema inamgharimu Sh2,000 tu kupata mkaa utakaomwezesha kupika, ingawa kwa sasa nao ni mdogo.

Lakini anapotakiwa kutumia gesi, amesema inamgharimu kati ya Sh27,000 hadi Sh28,000 kwa mara moja kujaza mtungi mdogo wa kilogramu sita.

Katika mazingira hayo, Omar anasema ni vema Serikali itazame upya suala hilo kuwarahisishia wananchi kutumia nishati safi.

“Nimekuja kununua mkaa wa Sh2,000, lakini ndo kama unavyoona ni kidogo sana, gesi ambayo ndiyo ilitakiwa tukimbilie na yenyewe imefikia Sh27,000 hadi Sh28,000 kwa mtungi mdogo. Mimi naona Serikali ilitazame hili kwa jicho la tatu,” anasema.

Habiba Kizugu mama lishe eneo la Mbagala Rangitatu anasema ili apike vizuri bila shida kwa siku hununua kuni za Sh14,000 na mkaa wa Sh800 hivyo akiwa na Sh22,000 anamaliza kuandaa chakula.

“Nikija kwenye gesiu ambayo tulipata elimu nikajaribu, hapa kwangu mtungi mdogo najidanganya nitahitaji walau wa kilo 15 ambao siwezi kuununua chini ya Sh50,000 kwa mara moja. “Tofauti ambayo wengi hawaisemi ni kwamba kuni na mkaa ninanunua kila siku kidogo kidogo na kwa mitaji ya mama lishe manunuzi tunafanya kila siku.”

“Gesi nitatakiwa ninunue kwa mara moja tena kwa gharama kubwa kwa mitaji yetu huku siyo rahisi, nakubaliana na wazo la matumizi ya nishati sana, kwanza inaokoa muda ila gharama zipo juu sana,”anasema Habiba.

Kambi Hijja muuza pweza eneo la Mtoni Kijichi anasema anatamani kutumia gesi kuanzia kundaa kachori hadi kuuza supu ya pwaze, lakini gharama ni kubwa hawezi kumudu.

“Hapa mbele yangu hao wauza chipsi wanatumia majiko ya gesi nawatamani sana, ila kwa mtaji wangu acha tu nibanane na mkaa, gharama za gesi au umeme siziwezi na vifaa pia sina,”anasema Hijja.

Akizungumzia matumizi ya gesi kupikia chipsi, kuku na mahitaji mengine, mfanyabishara Haji Kombo anayefanya shughuli zake Manzese anasema mbali ya kuivisha vyakula haraka pia anapata unafuu.

“Mimi nilikuwa ninatumia mkaa gunia moja siku mbili na wakati mwingine nalazimika kuongeza kidogo siku ya pili nikipata mkaa mbaya, lakini natumia gesi sasa kila kitu kipo sawa na faida ninapata.”

“Nakubali gesi ipo juu sana sana, lakini inanisidia ukilinganisha na nilipokuwa ninatumia mkaa, gharama na usumbufu wa kuwasha, kuongeza ongeza mkaa ila sasa sina pressha ya mkaa mbaya, kunamvua umelowa wala una chenga nitapata hasara,”anasema Kombo.

Matumizi zaidi ya mkaa kwa Watanzania yanathibitishwa katika Ripoti ya Uchumi wa Kanda wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) inayotolewa Machi kila mwaka, ikionyesha kuwapo ongezeko la mauzo ya mkaa na kuni.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, ‎Machi 2026 mauzo ya mkaa yaliongezeka na kufikia Sh7.8 bilioni ukilinganisha na Sh7.6 bilioni ya mwezi kama huo mwaka jana.

Kwa upande wa mauzo ya kuni Machi 2026, yaliongezeka na kufikia Sh150 milioni, ukilinganisha na Sh125.9 milioni ya mwezi huo mwaka jana.

‎‎Ukiacha takwimu hizo za mauzo ya kuni na mkaa, Kamishina Uhifadhi wa TFS, Profesa Dos Santos Silayo, aliiambia Mwananchi kuwa, Watanzania wengi wanatumia mkaa na kuni kama chanzo kikuu cha nishati ya kupikia.

Katika kulikabili hilo, anasema TFS imekuwa ikipandisha gharama za upatikanaji wa leseni ya biashara ya mkaa na kuni, lakini bado ni asilimia 30 tu ndiyo waliohamia kutumia nishati safi.

‎”Asilimia 70 bado wapo kwenye matumizi ya mkaa na kuni, tunajitahidi kupandisha gharama za leseni ili upatikanaji uwe mgumu pengine watu watahamia katika nishati safi,” anasema.

Vibali, leseni mkaa bei juu‎

Ili kuweka ugumu wa matumizi ya mkaa, Serikali imepandisha bei ya leseni na vibali vya kubeba nishati hiyo kutoka shambani, huku wafanyabiashara wakiomba nafuu kwa kuwa inawabana.

Mwenyekiti wa Soko la Mkaa Maliasili Gongolamboto, Hamis Duge, anaiomba Serikali ipunguze gharama za leseni na vibali vya kubeba mkaa kutoka shamba.

Anasema kwa sasa gharama za kibali cha kusafirisha kilo moja ya mkaa ni Sh260, kutoka Sh250 iliyokuwa ikitozwa awali. Sawa na ongezeko la Sh10.

‎”Vibali vimekuwa changamoto. Unaposajiliwa TFS ndipo unapata kibali cha kusafirisha mzigo. Kibali kwa gunia ni Sh28,000 ukiweka na usafiri Sh15,000 unajikuta gharama zinakuwa kubwa,” anasema Duge.

Katika Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, nishati safi imepewa nafasi muhimu katika kulinda mazingira. Serikali inalenga kupunguza utegemezi wa kuni na mkaa ili kukomesha ukataji miti, kuhifadhi bioanuwai na kuimarisha ustahimilivu dhidi ya mabadiliko ya tabianchi.

Dira hiyo pia inalenga kuhamisha matumizi nishati safi. Kupitia hatua hizo, Tanzania inakusudia kuwa kinara wa kikanda katika matumizi endelevu ya rasilimali za nishati na uhifadhi wa mazingira.‎

‎Akizungumzia hatua zinachochukuliwa na Serikali kuhusu suala hilo, Mkurugenzi wa Kitengo cha Nishati Safi ya Kupikia cha Wizara ya Nishati, Nolasco Mlay anasema wamepiga hatua kwa sababu matumizi ya nishati safi yamefikia asilimia 28.6 mwaka 2025 kutoka asilimia 6.9 mwaka 2021.

‎”Serikali inaendelea kutekeleza Mkakati wa Taifa wa Nishati Safi ya Kupikia wenye lengo la kuhakikisha asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034.

“Hatua mbalimbali zinaendelea kuchukuliwa, ikiwemo kuongeza upatikanaji wa gesi asilia, gesi ya kupikia (LPG) na umeme kwa ajili ya kupikia pamoja na teknolojia nyingine za nishati safi,” anasema Mlay.

Pia, anasema Serikali kupitia Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), inaendelea kutekeleza miradi ya kupanua matumizi ya gesi asilia kwenye makazi ya watu.

Katika mwaka wa fedha 2026/27, anasema nyumba 800 katika eneo la Kisemvule zimefanyiwa tathimini kwa ajili ya utekelezaji wa awamu ya pili ya mradi wa kusambaza gesi kwenye makazi ya watu unaofadhiliwa na Wakala wa Umeme Vijijini (REA).

‎”Unaendelea ujenzi wa miundombinu ya kusambaza na kuunganisha gesi asilia katika nyumba 1,000 jijini Dar es Salaam, katika maeneo ya Mikocheni A & B, Sinza, Lugalo na EACLC. Vilevile, katika mwaka wa fedha 2026/27, TPDC inalenga kufikisha huduma ya gesi asilia katika nyumba 800 mkoani Mtwara” anasema Mlay.

‎Anataja changamoto zinazopunguza kasi ya wananchi kuhamia kwenye matumizi ya gesi asilia ni gharama za kujenga na kupanua miundombinu ya usambazaji wa gesi.

Gharama zaidi, anasema ni kufikisha mabomba katika maeneo mapya, uwezo wa baadhi ya wananchi kumudu gharama za kuunganishwa na kununua vifaa vya kupikia kwa gesi.

‎”Katika kipindi cha miezi 12 ijayo, wananchi watarajie kuona  ujenzi na upanuzi wa miundombinu ya usambazaji wa gesi asilia ukiendelea, ikiwemo utekelezaji wa miradi ya kuunganisha nyumba 1,000 Dar es Salaam, pamoja na maandalizi ya kuunganisha nyumba 800 Kisemvule na nyumba 800 Mtwara” anasema.

Source link