Meatu. Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Said Mtanda amemtaka mkandarasi Sheree Company Limited kuongeza kazi ya ujenzi wa jengo la ghorofa moja la Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Meatu, unaosuasua licha ya Serikali kutoa fedha kwa mujibu wa mkataba.
Mtanda ametoa agizo hilo leo Alhamisi Oktoba 15, 2026, baada ya kupokea taarifa ya utekelezaji wa mradi huo wenye gharama ya zaidi ya Sh400 milioni, ikionyesha kuwa ujenzi umefikia asilimia 40, huku muda wa mkataba ukiwa umepita kwa siku 30.
Amesema agizo hilo linalenga kuhakikisha mkandarasi anaongeza kasi ya ujenzi na kukamilisha mradi kwa kuzingatia makubaliano ya mkataba, ili fedha za umma zilizotengwa kwa ajili ya kazi hiyo zitumike kwa malengo yaliyokusudiwa.
Mkuu wa mkoa wa Simiyu, Said Mtanda (aliye mbele) akiambatana na viongozi wengine akiwemo Mkuu wa wilaya ya Meatu,Grace Kingalame(wa kwanza kulia)wakikagua ujenzi wa jengo la ofisi ya Mkuu wa wilaya hiyo.Picha na Samwel Mwanga
“Kwa mujibu wa mkataba, jengo la ofisi lilipaswa kumalizika ujenzi wake mwezi mmoja uliopita. Sasa liko asilimia 40. Natoa siku 14 mkandarasi awe amemaliza ujenzi huu ili Mkuu wa Wilaya ya Meatu atoe huduma kwa wananchi,” amesema.
Awali, akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa mradi huo, Katibu Tawala Msaidizi anayeshughulikia miundombinu mkoani humo, Boniface William amesema miongoni mwa sababu za kusuasua kwa ujenzi ni mkandarasi kukosa fedha za kuendeleza kazi, licha ya Serikali kumlipa kwa mujibu wa mkataba.
Kwa upande wake, mwakilishi wa mkandarasi, Eligius Shayo amesema utekelezaji wa mradi huo umeathiriwa na changamoto za upatikanaji wa malighafi za ujenzi, zikiwemo saruji, pamoja na ugumu wa ardhi wakati wa uchimbaji.
Severine Dioniz, mkazi wa Mwanhuzi wilayani Meatu, amesema ni muhimu agizo hilo liambatane na ufuatiliaji wa karibu ili kuhakikisha mkandarasi anaongeza kasi ya kazi ndani ya muda aliopewa.
“Tunachotaka wananchi ni kuona ujenzi unaendelea kwa kasi na kukamilika. Muda wa mkataba umepita, hivyo ni muhimu kufuatilia kila hatua ili kujua kama mkandarasi anatekeleza alichoelekezwa,” amesema.
Mwonekano wa ujenzi wa jengo la ofisi ya Mkuu wa wilaya ya Meatu mkoani Simiyu ulipofikia kwa sasa. Picha na Samwel Mwanga
Naye Tito Shija, mkazi wa Mwanyahina, amesema kuchelewa kwa mradi huo kunaonyesha umuhimu wa kutatua changamoto za utekelezaji mapema badala ya kusubiri muda wa mkataba upite.
Chiku Mustapha, mkazi wa Mwamishali, amesema wananchi wanatarajia kuona maendeleo yanayoonekana katika ujenzi huo ndani ya siku 14 alizopewa mkandarasi.
Ametaka hatua zinazostahili zichukuliwe iwapo mkandarasi atashindwa kutekeleza wajibu wake kwa mujibu wa mkataba.
“Tunatarajia ndani ya siku hizo 14 kuwe na maendeleo yanayoonekana. Ikiwa mkandarasi atashindwa kutekeleza makubaliano, mamlaka husika zihakikishe hatua zinazotakiwa kwa mujibu wa mkataba zinachukuliwa,” amesema.


