Mafanikio ziara ya siku 10 ya Rais Mwinyi Ulaya

Mafanikio ziara ya siku 10 ya Rais Mwinyi Ulaya

Unguja. Ziara ya kikazi ya siku 10 ya Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Ali Mwinyi kimataifa, imetajwa kuleta mafanikio makubwa katika maeneo makuu manne ya diplomasia ya mazingira, michezo, elimu na uwekezaji.

Rais Mwinyi alianza ziara hiyo ya kimataifa Oktoba 7, 2026 katika nchi za Qatar, Uhispania na kuhitimishwa jijini Yerevan, Armenia.

Akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, Dk Mwinyi ameshiriki na kuhutubia Mkutano wa Viongozi kuhusu Bioanuai (COP17) jijini Yerevan, Armenia. 

Akizungumza katika mkutano huo Oktoba 16, Dk Mwinyi amesisitiza kuwa kulinda mazingira hakupaswi kuishia kwenye maneno pekee, bali kinachotakiwa ni hatua halisi za utekelezaji.

“Dhamira ya kimataifa ya kulinda bioanuai lazima iambatane na hatua halisi zinazohakikisha mifumo ya ikolojia inalindwa, inarejeshwa na kutumiwa kwa njia endelevu kwa manufaa ya wananchi na maendeleo ya uchumi,” alisema Dk Mwinyi.

Katika hotuba yake, alieleza kuwa Zanzibar imepanua hifadhi za bahari kutoka tano hadi saba, na kuongeza eneo la uhifadhi kutoka kilomita za mraba 2,400 hadi zaidi ya 3,600, ikiwemo maeneo mawili mapya kisiwani Pemba.

Zaidi ya hayo, alibainisha kuwa Tanzania inalenga kupata takriban Dola za Marekani 41 milioni kupitia mifumo ya kimataifa ya ufadhili wa mazingira ili kutekeleza miradi ya uhifadhi na urejeshaji wa mifumo ya ikolojia.

Katika hatua nyingine, Dk Mwinyi alikutana na Rais wa Armenia, Vahagn Khachaturyan, katika Ikulu ya Yerevan na kupendekeza ushirikiano wa kuanzisha kituo cha mafunzo ya teknolojia nchini Tanzania pamoja na ushirikiano wa kitalii na kidiplomasia.

Akijibu mapendekezo hayo, Rais Khachaturyan alisema Armenia iko tayari kuimarisha uhusiano na Tanzania katika sekta za utalii, elimu ya juu na akili mnemba (AI).

Rais Khachaturyan alieleza kwamba imetenga nafasi 50 za masomo katika vyuo vyake vya elimu ya juu kwa wanafunzi kutoka nchi za Afrika, na kuikaribisha Tanzania kunufaika na fursa hizo pamoja na programu za kubadilishana wanafunzi.

Pia, alibainisha kuwa Armenia imeanzisha kituo cha akili mnemba kwa ushirikiano na kampuni ya NVIDIA.

Real Madrid na Soka Zanzibar

Kabla ya kuwasili Armenia, Dk Mwinyi alifanya ziara nchini Uhispania ambapo alitembelea Makumbusho ya LEGENDS jijini Madrid na kushuhudia utiaji saini wa Hati ya Makubaliano (MoU) baina ya Real Madrid Foundation na Unicorn Zanzibar Sports Limited Oktoba 13, 2026.

Dk Mwinyi alisema ushirikiano huo utafungua fursa mpya kwa vijana wa Zanzibar kukuza vipaji vyao kwa kuunganisha michezo, nidhamu na maadili. 

Alieleza kuwa Serikali imeendeleza zaidi ya viwanja 30 vya mpira wa miguu Zanzibar na sasa inalenga kuleta maarifa ya kimataifa.

“Kipaji pekee hakitoshi kumfikisha kijana kwenye mafanikio bila mwalimu bora, nidhamu, elimu, miundombinu na mfumo unaotambua na kuendeleza uwezo wake,” alisisitiza Dk Mwinyi.

Naye, Mwenyekiti wa Unicorn Sports, Sergio Garcia alisema kampuni hiyo inalenga kuanza na mafunzo maalumu ya soka, yakifuatiwa na kuanzishwa kwa akademia ya kudumu katika Viwanja vya Michezo Zanzibar.

“Mpango huo utawaleta makocha wenye uzoefu kutoka Real Madrid kufanya kazi na makocha wa ndani watakaopatiwa mafunzo,” amesema.

Makamu Mwenyekiti wa Unicorn Sports, Mohamed Sleiman alisema matarajio yao ni kupanua wigo wa programu hiyo ili kuwafikia vijana wa kike na wa kiume kutoka maeneo mbalimbali ya Zanzibar, hususani wenye vipaji ambao bado hawajapata fursa za kuviendeleza.

Ziara nchini Qatar ilianza Oktoba 8, 2026, ambapo Dk Mwinyi alikutana na mfanyabiashara wa kimataifa, Omar Hussain Alfardan katika jengo la Alfardan Towers jijini Doha.

Katika mazungumzo hayo, Dk Mwinyi alihimiza uwekezaji katika sekta za utalii, hoteli, makazi na huduma za wageni.

Pia, Dk Mwinyi alitembelea mradi mkubwa wa makazi na biashara wa Kisiwa cha The Pearl (The Pearl Island) ulioko kwenye eneo la mita za mraba milioni nne lililofukiwa baharini, ukishikilia makazi 25,000 na wakazi 52,000. 

Akiwa katika jengo la The Oyster, alielezwa mpangilio na usimamizi wa mradi huo unaoendelezwa na United Development Company (UDC).

Ziara hii ya siku 10 ya Dk Mwinyi imedhihirisha dhamira ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya kuleta maendeleo endelevu, fursa za kiuchumi, michezo na teknolojia kwa wananchi wake kupitia ushirikiano wa kimataifa.

Source link