Dar es Salaam. Wanafunzi 264 wa Shule ya Msingi Buguruni Viziwi wameanza kunufaika na jiko la kisasa linalotumia nishati safi ya kupikia pamoja na alama za usalama barabarani, baada ya shule hiyo kuibuka mshindi wa kitaifa wa Mpango wa Usalama Barabarani wa VIA mwaka 2025.
Huduma hizo zimekabidhiwa na TotalEnergies Marketing Tanzania Limited kwa lengo la kuboresha usalama wa shule na mazingira yake.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa kampuni hiyo katika hafla iliyofanyika shuleni hapo leo Alhamisi, Septemba 3, Mkurugenzi wa Sheria na Mahusiano, Getrude Mpangile, amesema mpango huo unaonyesha mchango wa wanafunzi katika kuimarisha usalama wa jamii.
Muonekano wa jiko la zamani linalotumia Kuni lililopo katika Shule ya Buguruni viziwi. Picha na Jumanne Bakana.
Mpangile amesema tangu kuanzishwa kwa mpango huo mwaka 2022 kwa ushirikiano na TotalEnergies Foundation na Nafasi Art Space, umewafikia zaidi ya wanafunzi 32,000 katika shule 60 za Dar es Salaam, Morogoro, Dodoma na Pwani.
Amesema jiko hilo linaunga mkono Mkakati wa Serikali wa Nishati Safi ya Kupikia unaolenga kufikisha matumizi ya nishati hiyo kwa asilimia 80 ifikapo 2034.
Mkuu wa Dawati la Elimu Barabarani kutoka Makao Makuu ya Polisi, Mbunja Matibu, amepongeza uwekezaji huo kwa watoto wenye mahitaji maalumu na kutoa wito kwa sekta binafsi kuiga mfano huo.
Baadhi ya wanafunzi wa shule ya Buguruni viziwi wakiwa katika hafla ya uzinduzi wa jiko la gesi ikiwa ni sehemu ya tuzo ya shule hiyo, kuibuka mshindi wa kitaifa wa Mpango wa Usalama Barabarani wa VIA kwa mwaka 2025. Picha na Jumanne Bakana.
Mwalimu Mkuu Msaidizi wa shule hiyo, Richard Kweka, amesema awali wanafunzi walikuwa katika hatari ya ajali kutokana na ukosefu wa alama za kutosha, akieleza kuwa mwaka jana mwanafunzi mmoja aligongwa na pikipiki na kupoteza meno mawili.
Kweka ameomba mamlaka za barabara kuweka tuta eneo hilo ili kusaidia kupunguza mwendo wa magari.
Kuhusu jiko hilo, amesema limeongeza ufanisi katika mafunzo ya vitendo ya upishi, huku maji ya lita 60 sasa yakichemka kwa dakika 45, tofauti na ilivyokuwa kwa matumizi ya kuni.


