Namtumbo. Wajasiriamali wakiwamo Mama Lishe Wilayani Namtumbo, Mkoa wa Ruvuma, wameshauriwa kuachana na matumizi ya kuni na mkaa na badala yake kutumia nishati safi ya kupikia kwa ajili ya kulinda afya zao na mazingira.
Ushauri huo umetolewa leo Ijumaa Septemba 18, 2026, na Meneja Fedha wa Kampuni ya Oryx Gas, Ashery Mbasha, aliyemwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa kampuni hiyo, Iman Mtafya.
Mbasha amekabidhi mitungi 600 ya gesi na vifaa vyake vilivyotolewa na kampuni ya Oryx kwa kushirikiana na Mbunge wa Namtumbo, ambaye pia ni Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Juma Homera.
Akizungumza katika hafla hiyo, amesema ili kufikia lengo la Serikali la kuhakikisha angalau asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo 2034, ni muhimu kuendelea kuhamasisha matumizi ya nishati hiyo.
Amesema Oryx Gas imekuwa mstari wa mbele katika kampeni ya kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini.
“Wilaya ya Namtumbo, kama yalivyo maeneo mengine hapa nchini, imekuwa na changamoto ya matumizi makubwa ya kuni na mkaa kwa muda mrefu. Hili limekuwa chanzo kikubwa cha uharibifu wa misitu na iwapo hatua madhubuti hazitachukuliwa, zitasababisha athari kubwa, ikiwemo mabadiliko ya tabianchi,” amesema.
Amesema Serikali imedhamiria kuhakikisha kila Mtanzania anatumia nishati safi ya kupikia.
“Sisi tumeanza na ninyi Mama Lishe kwa sababu nyinyi ndio mnaotumia kuni nyingi zaidi na ndio mnaoathirika zaidi na moshi,” amesema.
Mbasha amesema matumizi ya gesi ya kupikia yatasaidia kupunguza kasi ya ukataji miti, kuboresha afya za wananchi kwa kupunguza athari za moshi, kuokoa muda wa kupika na kuongeza ubora wa maisha kwa ujumla.
“Dhamira ya Oryx Gas ni kuhakikisha Tanzania inafikia mabadiliko kamili ya matumizi ya nishati safi ya kupikia, akieleza kuwa Namtumbo ni miongoni mwa maeneo ambayo kampuni hiyo imeyaweka katika vipaumbele vyake,” amesema Mbasha.
Aidha, amewataka wananchi wa Namtumbo, hasa waliopatiwa mitungi ya gesi ya Oryx, kutumia majiko hayo kwa usalama na kuendelea kutoa elimu kuhusu matumizi salama ya gesi ya LPG katika jamii zao.
“Kwa pamoja tunaweza kujenga Namtumbo yenye mazingira bora, afya bora na maendeleo endelevu,” amesema.
Awali, Mbunge wa Namtumbo, Dk Homera ameishukuru Oryx Gas kwa kuwapatia wananchi mitungi na majiko hayo, akisema Rais Samia Suluhu Hassan, ambaye amesema ni kinara wa nishati safi ya kupikia, amekuwa akisisitiza matumizi ya nishati hiyo nchini.
Dk Homera amewataka wananchi kuunga mkono kwa vitendo jitihada za Rais na Serikali ya Awamu ya Sita katika kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Pia ameipongeza kampuni hiyo kwa ushirikiano inaoutoa kwa wananchi wa Namtumbo.
Kwa upande wake, Mama Lishe, Anifa Mahela amepongeza mpango huo wa kutoa elimu na kugawa bure mitungi ya gesi kwa wajasiriamali.
Hata hivyo, ameiomba Serikali na wadau, wakiwemo Oryx Gas, kuwasaidia wajasiriamali kupata mitungi ya gesi na majiko ya nishati safi kwa bei ya ruzuku kutokana na kuwa na mitaji midogo.


