Unguja. Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Othman Masoud Othman amesema maridhiano ya kisiasa yaliyofikiwa Zanzibar ni sehemu ya mafundisho mema ya dini ya Kiislamu, yanayohimiza haki, umoja, mshikamano na amani katika jamii.
Othman ameyasema hayo leo Oktoba 16, 2026, alipokuwa akizungumza na waumini wa Kiislamu baada ya kushiriki sala ya Ijumaa katika Msikiti wa Makuti, Jang’ombe, Mkoa wa Mjini Magharibi, Unguja.
Amesema Uislamu hauishii katika kutekeleza ibada misikitini, bali unamtaka muumini kuishi kwa kufuata maadili na mafundisho yake katika maisha ya kila siku, ikiwemo kusimamia haki na kuepuka migogoro.
“Uislamu siyo tu kuja msikitini na kurudi, bali kuyatenda yale yote mema yaliyomo ndani yake, ikiwemo kushikamana na haki na kuepuka migogoro,” amesema Othman.
Amesema iwapo jamii itayatumia ipasavyo mafundisho ya dini ya Kiislamu, dunia itakuwa mahali salama zaidi, penye umoja, mshikamano na upendo miongoni mwa watu.
Akizungumzia suala la ushindani, Othman amesema ni sehemu ya maisha ya mwanadamu, lakini unapaswa kuendeshwa kwa misingi ya amani na kuheshimiana, badala ya kutumia njia zinazowaumiza wengine ili kupata nafasi au mamlaka.
“Tushindaneni katika hali ya amani ili ashindaye atawale kwa amani, na siyo kutumia hila na mabavu, jambo ambalo husababisha machafuko na ukosefu wa amani,” amesema.
Kwa upande wake, Khatib wa sala hiyo, Sheikh Salim Muridu Fakih amewataka waumini kuongeza ibada kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu, kufuata mafundisho mema ya Mtume Muhammad (S.A.W.) na kujiepusha na maovu.
Sheikh Muridu amesema kumcha Mungu wa kweli unapaswa kuonekana katika matendo mema, upendo, umoja na utayari wa kuleta maridhiano pale watu wanapokoseana, huku akisisitiza umuhimu wa kulinda amani katika jamii.
“Ucha Mungu wetu utatimia pale tutakapotenda mema, tutakapoungana na kuwa wamoja, tutakapopendana, tutakapoleta maridhiano tukikoseana, pamoja na kuleta na kutunza amani,” amesisitiza.


