Dodoma. Mpango wa Kisiki Hai umeanza kuboresha maisha ya wakulima katika maeneo yenye ukame nchini kwa kurejesha miti ya asili, kuimarisha rutuba ya ardhi na kuongeza mavuno, huku wakulima wakinufaika pia na upatikanaji wa kuni na malighafi za ujenzi.
Akizungumza na Mwananchi hivi karibuni, Mwamini Kutosha, mkulima katika Kijiji cha Mkondai, Wilaya ya Bahi alisema mavuno kwenye shamba analopanda mazao mchanganyiko yameongezeka kutoka magunia mawili hadi 13 katika eneo la ekari saba.
Amesema hiyo ni baada ya kuanza kutunza miti inayochipua kwenye visiki na kutumia mbinu za kuhifadhi udongo na maji.
“Zamani ardhi haikuwa na rutuba na tulikuwa tunapata mavuno kidogo. Sasa miti imesaidia kupunguza mmomonyoko wa udongo na hali ya shamba imebadilika,” amesema Mwamini.
Amesema mbali na kuimarisha hali ya mashamba, miti hiyo inampa kuni na malighafi za kutengeneza mkaa, hivyo kupunguza utegemezi wa misitu ya hifadhi kwa mahitaji ya nishati ya nyumbani.
Kisiki Hai ni mbinu ya kurejesha uoto wa asili kwa kuhifadhi machipukizi yanayoota kwenye visiki na mizizi ya miti iliyokatwa au kuharibika, lakini ikabaki hai.
Katika mbinu hiyo, mkulima huchagua machipukizi yanayofaa, kuyaacha yakue na kuyapogoa ili miti iendelee kukua bila kuathiri uzalishaji wa mazao shambani.
Tofauti na kupanda miche mipya, Kisiki Hai hutumia mizizi ya miti iliyokomaa na kuendelea kuwa hai ardhini. Hali hiyo husaidia kupunguza gharama za kununua miche na umwagiliaji wakati wa kuanzisha miti mipya.
Mpango huo unatekelezwa na shirika la LEAD Foundation kwa kushirikiana na Justdiggit katika mikoa ya Dodoma, Singida, Arusha na Manyara, ambako uharibifu wa ardhi na upotevu wa miti ni miongoni mwa changamoto zinazoathiri shughuli za kilimo na ufugaji.
Mkurugenzi wa Programu wa LEAD Foundation, Njamas Chiwanga, amesema awamu ya kwanza ya mpango huo, iliyoanza mwaka 2017, imewezesha kurejeshwa kwa miti zaidi ya milioni 32.3 kupitia mbinu ya Kisiki Hai.
Amesema wakulima vinara zaidi ya 3,000 wamepatiwa mafunzo ili kuwasaidia kusambaza ujuzi huo kwa wakulima wengine katika jamii zao.
“Kwa kawaida Kisiki Hai haina gharama kubwa. Mtu anaangalia visiki vinavyochipua, anachagua miti anayoitaka na kuipogoa. Baada ya hapo miti inaendelea kukua,” anasema Chiwanga.
Kwa mujibu wa Chiwanda, mafanikio ya mbinu hiyo yanatokana na matumizi ya miti ya asili inayoendana na mazingira ya eneo husika, pamoja na uwepo wa mizizi iliyokomaa na kujijenga ardhini.
Meneja Mkazi wa Justdiggit Tanzania, Mary Sengelela amesema awamu ya pili ya mpango huo inalenga kurejesha hekta milioni moja za ardhi na kufikisha miti milioni 100 ifikapo mwaka 2030.
Amesema katika kuchagua vijiji vitakavyonufaika na mpango huo, huzingatia uwepo wa visiki vyenye uwezo wa kuchipua, ushirikiano wa viongozi wa maeneo husika na utayari wa wakulima kujifunza na kuwafundisha wengine.
“Baada ya mafanikio ya awamu ya kwanza, tumeona umuhimu wa kuongeza kasi. Utunzaji wa miti mashambani umechangia kuboresha ardhi na kuongeza fursa za kipato kwa wakulima,” anasema Sengelela.
Katika Kitongoji cha Punga, mkulima Lucas Chipang’a anasema awali alikuwa na mashaka kuhusu kuacha miti ikue ndani ya mashamba yake, akihofia kuwa ingeathiri uzalishaji wa mazao.
Hata hivyo, baada ya kupata mafunzo mwaka 2018, alianza kutunza machipukizi ya miti na sasa ana takribani ekari 12 zenye miti iliyorejeshwa kwa kutumia mbinu hiyo.
Ofisa Misitu Mwandamizi kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais, Timoth Mande, amesema Kisiki Hai inaonyesha namna jamii zinavyoweza kurejesha uoto wa asili kwa gharama nafuu huku zikiboresha mazingira na kusaidia shughuli za uzalishaji.
Amesema moja ya changamoto katika utekelezaji wa mbinu hiyo, ni kulinda machipukizi dhidi ya moto na mifugo inayochungwa kiholela.
Kutokana na hali hiyo, amesisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya serikali za vijiji na wakulima katika kusimamia uhifadhi wa miti na matumizi bora ya ardhi.
Mwamini pia anataja mifugo inayoingia mashambani kuwa tishio kwa miti michanga, akiiomba serikali ya kijiji kusimamia matumizi ya ardhi ili kulinda miti hiyo na kuhakikisha inaendelea kukua.


